Taasisi ya Volunteers In Development (VID) imefanya matembezi ya hisani
kwa ajili ya kuchangia mahitaji ya shule kwa watoto yatima wa majumbani
zaidi ya 850 tarehe 5 Disemba 2021.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Nishati na Madini Mhe.Januari
Makamba amesema jamii inapaswa kushiriki katika matukio mbalimbali
yanayolenga kuleta maendeleo kwa watu wenye uhitaji ili kuondokana na
changamoto zinazoweza kuvunja amani.
“Nawasihi kuendelea kuombea nchi yetu iwe na amani na utulivu na
kudumisha moyo wa utoaji kwa wenye uhitaji, kwani tutaondoa matabaka kwa
kuwafanya wasio nacho wasione wametengwa na mwisho wa siku wakaingia
katika vitendo viovu” amesema.
Amesema kupitia matembezi hayo wataweza kuwafikia watoto kupata
mahitaji yao kwani kuna umuhimu mkubwa wa kupata haki ya elimu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa VID Tune Shaabani amesema elimu ni
kipaumbele kikubwa cha VID ili kuleta maendeleo na mabadiliko chanya kwa
jamii.
“Kila ifikapo mwisho wa mwaka huwa tunafanya zoezi la harambee kuwapatia
mahitaji ya shule kama kalamu, madaftari, sare za shule, mabegi na mahitaji
yote. Elimu ni kipaumbele kikubwa kwetu kama tunavyojua kuwa elimu ni
bure Tanzania ila kuna gharama mbalimbali za kuendesha elimu hiyo”
amesema.
Amesema jamii ikishikana kumuendeleza mtoto yatima kielimu itakuwa
msaada mkubwa kuleta maendeleo na mabadiliko makubwa katika taifa,
kwani atakuwa na nafasi nzuri ya kuisaidia familia yake na jamii yake kwa
kupambana dhidi ya umasikini na ujinga.
Taasisi ya VID ni taasisi ya kinamama ambayo imedhamiria kuleta mabadiliko
chanya katika jamii kwa kuelekeza nguvu kuwasaidia watoto yatima wa
majumbani, wajane na wasiojiweza ambapo katika zoezi la matembezi ya
hisani yalilenga kuwafikia watoto zaidi ya 865 katika mahitaji ya elimu.
Latest news delivered right to your inbox!
Leave a Reply